Lugha Nyingine
Kiongozi wa Palestina Abbas atoa wito wa juhudi za kukomesha ukaliaji kimabavu, "mauaji ya halaiki" ya Israel kwenye mkutano wa UNGA
Rais wa Palestina Mahmoud Abbas akitoa hotuba katika Mjadala Mkuu wa mkutano wa 79 wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa (UNGA) kwenye makao makuu ya Umoja wa Mataifa mjini New York, Septemba 26, 2024. (Xinhua/Li Rui)
UMOJA WA MATAIFA - Rais wa Palestina Mahmoud Abbas amepigiwa makofi ya pongezi kwa muda mrefu alipokuwa akihutubia Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa (UNGA) siku ya Alhamisi, akisisitiza kwamba "hatutaondoka, Palestina ni ardhi yetu," na "kama kuna yeyote anayepaswa kuondoka basi ni mkaliaji kimabavu."
Ameendelea kuishutumu Israel kwa kuendeleza "vita kamili vya mauaji ya halaiki," akitupilia mbali madai ya Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu kwamba Israel haikuua raia huko Gaza. "Nakuuliza, ni nani basi aliyeua watoto zaidi ya 15,000?" amesema.
"Komesha uhalifu huu. Komesha sasa. Komesha kuua watoto na wanawake. Komesha mauaji ya halaiki. Komesha kupeleka silaha kwa Israeli. Ujinga huu haupaswi kuendelea. Dunia nzima inawajibika kwa kile kinachotokea kwa watu wetu," Abbas amesema.
Vikwazo na Kutenga
Kwenye hotuba yake hiyo, Abbas ametoa wito kwa jumuiya ya kimataifa kuiwekea Israel vikwazo na pia kutengwa na Umoja wa Mataifa kufuatia "mauaji ya halaiki huko Gaza."
"Tunatoa wito wa vikwazo dhidi ya Israel. Israel haistahili kuwa sehemu ya shirika hili. Sijui ni kwa vipi Marekani inaweza kusisitiza kutunyima haki zetu," Abbas amesema, akiongeza kuwa Israel lazima inyang'anywe uanachama wa Umoja wa Mataifa kwa kushindwa kukubali azimio la kuunda nchi mbili kwa mgogoro huo na kuruhusu kurudi kwa wakimbizi wa Palestina kwenye makazi yao. "Tutawasilisha ombi kwenye UNGA kuhusu suala hili," amesema.
Uhalifu na Mauaji ya Kimbari
Akisisitiza kwamba Wapalestina wamestahimili karibu mwaka mmoja wa kile alichokiita kuwa moja ya jinai mbaya zaidi ya nyakati hizi, kiongozi huyo amesema "ni uhalifu wa vita kamili vya mauaji ya halaiki ambavyo Israeli inaendesha. Uhalifu ambao umeshaua mashujaa zaidi ya 40,000 mjini Gaza pekee, na maelfu wengine wanaendelea kuwa chini ya vifusi. Uhalifu ambao umeshajeruhi watu zaidi ya 100,000 hadi leo.
Rais wa Palestina Mahmoud Abbas akitoa hotuba katika Mjadala Mkuu wa mkutano wa 79 wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa (UNGA) kwenye makao makuu ya Umoja wa Mataifa mjini New York, Septemba 26, 2024. (Xinhua/Xie E)
Rais wa Palestina Mahmoud Abbas (kwenye mimbari na kwenye skrini) akitoa hotuba katika Mjadala Mkuu wa mkutano wa 79 wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa (UNGA) kwenye makao makuu ya Umoja wa Mataifa mjini New York, Septemba 26, 2024. (Xinhua/Xie E)
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma